Share

Utalii Songea waporomoka/ Selebuka Festival yatinga milima ya ajabu ya Matogoro

Share This:

INGAWAJE serikali ya Mkoa wa Ruvuma imetoa fursa kwa wananchi wake kutembelea vivutio vilivyomo mkoani humo, bado mwamko wa wananchi ni hafifu, huku Tamasha la Majimaji Selebuka likipewa heko na Mkuu wa Wilaya wa Songea, Poreleti Kamando kwani limekuja kubadili ‘upepo’.
Takwimu zinaonesha kwa mwaka wastani wa kupokea watalii ni mara kumi tu, licha ya mkoa wa Ruvuma kujaaliwa utitiri wa vivutio vya kitalii asilia, kama vile Misitu minene ya Matogolo, chanzo cha mto Ruvuma kilichopo mpangilio ya milima ya Matogolo, mabawa ya samaki, makumbusho ya Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Rashid Kawawa, Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji 1905 na vingine vingi.
DC Kamando amepongeza Taasisi ya So-Mi ambayo huratibu Tamasha la Majimaji Selebuka kila mwaka ambalo mbali na shughuli nyingine, sekta ya utalii imepewa kipaumbele zaidi kama njia ya kuhamasisha utalii wa ndani.
“Katika kutangaza utalii, tamasha hili limekuwa likiisaidia serikali kutekeleza ilani ya serikali ya sasa, ili kupitia vyombo vya habari Tanzania nzima iweze kujua vivutio vilivyopo Ruvuma na kusini mwa Tanzania kwa ujumla.
“Tunaamini kupitia tamasha hili, watu watavutika na watatembele vivutio vyetu na hawahawa watakuwa mabalozi huko waendako.
“Kwa niamba ya serikali, nawashukuru kwani mnatutendea mema na kutekeleza yale yaliyo kwenye mipango ya serikali yetu na hii inatupa nafasi ya kutangaza fursa ya utalii tulionayo Ruvuma,” alisema Kamando.
Kwa mwaka huu, ziara ya utalii wa ndani ilikuwa kwenye misitu minene ya milima ya Matogolo pamoja na kwenye chanzo kikuu cha Mto Ruvuma kilichopo nyanda za juu kwenye milima ya mpangilio ya Matogolo.
Kwa mujibu wa Lekoko Olenjilalo, Muhifadhi Misitu msaidizi mkoa wa Ruvuma, alisema wastani wa kupokea watalii kwa mwaka ni mara kumi.
“Ukweli mwamko ni mdogo, pamoja na kwamba hakuna kiingilio lakini bado. Wastani kwa mwaka utakuwa tunapokea watalii mara kumi hadi kumi tano na asilimia kubwa ni viongozi tu, kwa wananchi wa kawaida suala la utalii kwao bado,” alisema Lekoko.
Profesa Julian Murchison, raia wa Marekani ni miongoni mwa waliokwenda kutalii milima ya Matogolo: “Hii ni safari yangu ya kwanza kufika hapa, ila nimefurahi sana kuona mazingira ya hivi (mwamba mweupe kileleni mwa milima ya Matogolo). Mazingira yanavutia, kuna upepo mzuri kileleni na pia kuona chanzo cha mto mkubwa (Ruvuma), inapendeza kwa kweli.”

Leave a Comment