Share

MTANZANIA AKUTWA NA KUCHA ZA SIMBA, MENO ABURUTWA KORTINI “MIL.113, MAKUMBUSHO “

Share This:

Mtanzania Emmanuel Ndossy amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo la kumiliki kucha za Simba 93 na meno 25 bila kibali vyenye thamani ya Sh Mil 113.1.

Ndossy (30) ambaye ni Mkazi wa Makumbusho amefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kassian Matembele.

Baada ya kusomewa mashitaka yake mshitakiwa huyo ameunganishwa na washitakiwa wenzake 7 ambao walishafikishwa Mahakamani hapo.

Washitakiwa hao saba ni pamoja na Hamis Rashid (27),James Kilanga (29), Mussa Bakari (39), Masoud Athumani (55), Abdillahi Ngunula (53), Sweetbert Mnembuka (34), pamoja na Milkaely Mayoni (25).

Kupitia hati ya Mashitaka Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon alidai mshitakiwa huyo pamoja na wenzake walikabiliwa na Mashitaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukutwa na nyara za Serikali bila kibali na Utakatishaji fedha.

Shitaka la kwanza, Wakili Simon alidai tarehe tofauti kati ya Machi, mwaka 2020 na Desemba 14, 2020 maeneo tofauti ya Dar-es-Salaam na Lindi mshitakiwa Ndossy na wenzake waliongoza genge la uhalifu.

Katika Shitaka la pili ni kukutwa na nyara za Serikali bila kibali.

Ilidaiwa, Desemba 14, mwaka 2020 eneo la Kinondoni jijini Dar-es-Salaam mshitakiwa huyo na wenzake 7 walikutwa wakimiliki kucha 93 za Simba na meno 25 vyenye thamani ya Sh Mil 113,145,410 bila kuwa na kibali kutoka kwa kamishna wa wanyamapori.

Shitaka la tatu ni utakatishaji fedha kiasi cha Sh Mil 113,145,410 ambapo wakili Simon alidai Desemba 14, 2020 eneo la Kinondoni Machungwa wilayani Kinondoni jijini Dar-es-Salaam mshitakiwa huyo na wenzake (Rashid,Kilanga,Bakari, Athumani,Ngunula, Mnembuka na Mayoni) walijipatia meno na kucha hizo wakati wakijua ni zao la makosa tangulizi ya kuongoza genge la uhalifu (uwindaji haramu).

Baada ya kusomwa kwa Mashitaka hayo wakili Simon alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ambapo kesi hiyo ilipangwa tena Januari 18, 2021.

Mshitakiwa Ndossy amerudishwa rumande baada ya Mashitaka yake kutokuwa na dhamana.

Leave a Comment